Taarifa ya Faragha
Toleo la 2026-09-18
Taarifa hii inaeleza taarifa binafsi tunazokusanya kwenye Kodi, kwa nini tunazikusanya, nani anaziona, na haki ulizo nazo chini ya Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi ya Tanzania ya mwaka 2022.
Nani anahusika na taarifa zako
Kama wewe ni mpangaji: mwenye nyumba au wakala unayepanga kwake ndiye mwenye dhamana ya taarifa zako. Yeye ndiye aliyeamua kuzikusanya na ndiye unayemwuliza. Kabolik Company Ltd, kampuni inayomiliki Kodi, ni mchakataji tu — tunazihifadhi kwa maelekezo yake.
Kama wewe ni mwenye nyumba au mtumishi aliyealikwa: Kabolik Company Ltd ndiye mwenye dhamana ya taarifa za akaunti yako — jina, namba ya simu, barua pepe, kumbukumbu za matumizi na ukaguzi — na haki zako unazitumia dhidi yetu.
Tunakusanya nini
- Utambulisho: jina, namba ya simu, namba ya NIDA, kazi, na hati za utambulisho unazopakia.
- Upangaji: fremu au uniti unayopanga, muda wa mkataba, masharti, mashahidi na saini.
- Fedha: kodi na gharama za huduma, malipo uliyofanya, risiti na madeni.
- Mawasiliano: kumbukumbu za SMS tulizokutumia na simu za ufuatiliaji zilizorekodiwa.
Kwa nini tunazikusanya
- Kwa ajili ya mkataba: utambulisho na kumbukumbu za malipo zinahitajika ili mkataba wa kupanga uwepo na ufuatiliwe. Hizi haziwezi kuondolewa wakati mkataba unaendelea.
- Kwa ridhaa yako: ujumbe wa matangazo pekee. Unaweza kuondoa ridhaa wakati wowote, na tutasimamisha mara moja bila swali.
- Kwa matakwa ya sheria: kumbukumbu za fedha tunazotakiwa kuzihifadhi na sheria za kodi.
Nani anaziona
Mwenye nyumba na watumishi aliowapa ruhusa pekee. Msimamizi anaona fremu na uniti alizopangiwa tu na hawezi kusoma namba yako ya NIDA. Mhasibu anaona fedha bila utambulisho. Hatuziuzi wala kuzikodisha kwa mtu yeyote.
- Watoa huduma za ujumbe wanaopeleka SMS na WhatsApp kwa niaba ya mwenye nyumba — NextSMS, na WhatsApp Cloud API inayoendeshwa na Meta. Wanapokea namba ya simu na maandishi ya ujumbe.
- Mtoa huduma wa barua pepe anayepeleka namba za uthibitisho kwa watumishi — Resend. Anapokea anwani ya barua pepe ya mtumishi na maandishi ya namba hiyo. Taarifa za mpangaji hazifiki kwake kamwe.
- Mtoa huduma wa seva anayehifadhi mifumo yetu, na pale sheria, amri ya mahakama au mamlaka ya udhibiti inapotulazimu.
Wafanyakazi wa Kabolik hawawezi kupitia taarifa zako. Hakuna mwonekano wa kiutawala unaovuka mashirika. Timu ya msaada ikihitaji kuingia, lazima iombe, mwenye nyumba akubali ndani ya mfumo, na ruhusa hiyo inaisha yenyewe baada ya saa mbili na inarekodiwa yote.
Taarifa zako zinahifadhiwa wapi
Kwa sasa zinahifadhiwa nje ya Tanzania, kwenye miundombinu iliyoko Umoja wa Ulaya, kwa muda wa majaribio haya ya awali. Maombi ya kibali cha kuhamisha taarifa nje ya nchi yapo kwa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) na bado hayajaidhinishwa. Zitarudi Tanzania, kwenye kituo cha seva Dar es Salaam, mkataba utakapokamilika.
Zaidi ya mahali zinapohifadhiwa, kuna njia mbili za ujumbe zinazotoka nje ya Tanzania. Ya kwanza: ujumbe unapotumwa kwa WhatsApp, namba ya simu na maandishi yake hushughulikiwa na Meta Platforms nje ya Tanzania. Ujumbe wa SMS kupitia NextSMS hubaki ndani ya Tanzania.
Ya pili: namba ya uthibitisho inayotumwa kwa barua pepe hushughulikiwa na Resend nje ya Tanzania. Hii inawahusu watumishi wanaoingia kwa barua pepe pekee; hakuna taarifa ya mpangaji inayopita njia hii.
Tunazihifadhi kwa muda gani
Kumbukumbu za fedha huhifadhiwa kwa muda unaotakiwa na sheria za kodi. Taarifa nyingine huhifadhiwa kwa muda mkataba wako unaendelea na kipindi ambacho mwenye nyumba amekiweka baada ya kuondoka. Muulize mwenye nyumba wako kipindi alichokiweka.
Haki zako
- Kuomba nakala ya taarifa zote tulizo nazo kukuhusu.
- Kuomba marekebisho ya taarifa isiyo sahihi.
- Kuomba taarifa zako zifutwe pale ambapo hakuna mkataba unaoendelea wala deni au sharti la kisheria linalotulazimu kuzihifadhi.
- Kuondoa ridhaa ya ujumbe wa matangazo wakati wowote, huku risiti na taarifa za mkataba zikiendelea kufika.
Jinsi ya kuomba
Mwambie mwenye nyumba au wakala wako. Ana kitufe ndani ya Kodi cha kufungua ombi lako, kulithibitisha na kukupa jibu — na kila hatua inarekodiwa.
Vidakuzi na taarifa kwenye kifaa
Kodi huweka kidakuzi cha kikao ili ubaki umeingia. Ni cha lazima; mfumo hauwezi kufanya kazi bila hicho.
Pia huweka kidakuzi cha lugha kinachokumbuka kama ulichagua Kiswahili au Kiingereza. Hatutumii vidakuzi vya matangazo wala vifuatiliaji vya nje.
Ukisakinisha Kodi kwenye simu yako, sehemu ya kazi zako huhifadhiwa kwenye kifaa ili ifanye kazi bila mtandao. Namba za utambulisho, hati za utambulisho na PDF za mikataba hazihifadhiwi kamwe kwenye kifaa. Ukifuta taarifa za kivinjari au ukitoka, nakala hiyo inaondoka.
Kwa wenye nyumba: masharti ya uchakataji
Kama unashikilia usajili wa Kodi, wewe ni mdhibiti wa taarifa na Kabolik ni mchakataji. Masharti yanayotufunga — maelekezo, usiri, usalama, wachakataji wadogo, uvunjaji wa taarifa na ufutaji — yako Sehemu B ya hati kamili ya Taarifa ya Faragha, na ni sehemu ya Masharti ya Matumizi.
Malalamiko na mawasiliano
Kabolik Company Ltd, Na. 11, Kijitonyama, Dar es Salaam. Barua pepe: legal@kodi.co.tz. Kama hukuridhika na jibu, unaweza kupeleka malalamiko kwa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) ya Tanzania.